Main Article Content

Ukopaji kama mkakati wa kuendeleza istilahi za tehama katika Kiswahili: uchanganuzi wa vidahizo teule vya Kamusi Sanifu ya Kompyuta (2011)


Stanley Adika Kevogo

Abstract

Kadiri jamii inavyokua katika usasa, ndivyo leksikoni inayotumika kuelezea shughuli mbalimbali inavyotanuka kwa kutumia mikakati anuwai kwenye mfumo wa lugha mahususi kuundia maneno mapya. Mojawapo ya mikakati hiyo ni ukopaji wa maneno. Makala hii inachunguza maneno mkopo katika uwanja wa istilahi za Kiswahili zinazotumika katika kompyuta. Azma kuu ni kutathmini aina na namna ukopaji unavyotekelezwa kuundia istilahi za Kiswahili zinazotumika katika kompyuta. Malengo ya utafiti huu ni kuchambua aina za ukopaji na jinsi unavyojitokeza, kuchanganua vipengele vya kimuundo vya istilahi mkopo na kueleza upungufu unaodhihirika katika taratibu za kuundia istilahi mkopo. Kimsingi, huu ni utafiti wa maktabani uliotekelezwa kwa mikabala ya kitaamuli na kitakwimu. Sampuli ya vidahizo 1096 iliteuliwa kwa uteuzi mpango kutoka katika vidahizo 3286 vya Kamusi Sanifu ya Kompyuta. Istilahi zilizokusanywa ziliainishwa katika makundi na kuchanganuliwa. Uchanganuzi wa istilahi hizo ulitekelezwa kwa mujibu wa vigezo vya istilahi faafu vya PEGITOSCA katika Nadharia ya Istilahi za Kisayansi (NIK). Matokeo ya uchunguzi yalidhihirisha kwamba kati ya aina tatu za ukopaji: utohozi, uasilishaji na tafsiri mkopo, ni tafsiri mkopo ndiyo iliyochangia idadi kubwa zaidi ya mikopo. Hali hiyo ilihusishwa na uundaji wa istilahi kwa mikakati ya upili. Faharasa ya istilahi za Kiingereza iliandaliwa na wanaistilahi waliozihawilisha kwa Kiswahili. Ukopaji umebainika kupungukiwa kwa sifa za uzalishi na uangavu. Maumbo mengi ya kigeni yalihawilishwa kwa Kiswahili bila kubaini maana za mofu wala kuzingatia mifumo ya dhana. Inapendekezwa kwamba mchakato wa uundaji istilahi uanze kwa mkakati wa ukopaji. Wanaistilahi wakope istilahi kama hatua ya awali kuelekea kwenye uzingatiaji wa mifumo ya dhana.


Journal Identifiers


eISSN: 2591-7013
print ISSN: 2665-0789