Main Article Content

Matumizi ya misimu kwa wazungumzaji wa Kiswahili katika vyuo vikuu nchini Tanzania: uchunguzi kifani wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere


Editha Adolph

Abstract

Makala hii inachunguza matumizi ya misimu kwa wazungumzaji wa Kiswahili katika vyuo vikuu nchini Tanzania, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kikichukuliwa kama mfano unaowakilisha vyuo vingine. Data za makala hii zimekusanywa kwa kutumia mbinu za uchambuzi wa matini, hojaji na usaili. Mbinu ya kuchambua matini ilijumuisha usomaji wa majarida, nyaraka za kitaaluma mathalani, tasinifu, kamusi na nyaraka zinazohusiana na mada husika. Aidha, mbinu ya hojaji ilijumuisha hojaji, ambapo ziligawiwa kwa wanachuo 20 wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambacho kinapatikana katika Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam. Aidha, mtafiti ametumia usaili kama mbinu nyingine ya kupata data ya makala hii. Nadharia iliyoongoza makala hii ni Nadharia Jumuishi ya Giles (1979). Halikadhalika, mkabala wa kitaamuli au maelezo ulitumika kuchambulia data ya makala hii. Licha ya suala la misimu kuangaziwa na Malima (2018) ambaye alichunguza misimu inayotumiwa na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Mkoa wa Morogoro katika mitandao ya kijamii, bado kuna haja ya kuangazia suala hilo katika vyuo vikuu kwa kutumia mazingiria na muktadha mwingine tofauti, wa kuchunguza matumizi ya misimu katika mawasiliano ya wanafunzi ya kawaida wakiwa katika mazingira ya Chuo Kikuu na sio katika mitandao ili kujua kinagaubaga aina ya misimu inayoibuliwa. Matokeo yameonesha kuwa misimu inayotumiwa na wanachuo hao hupatikana katika nyanja mbalimbali: taaluma, uchumi pamoja na jamii. Maana ya misimu hiyo imeoneshwa kutokana na majibu ya watoa taarifa wa makala hii. Makala hii inapendekeza vyombo vinavyosimamia Kiswahili (k.v. BAKITA na BAKIZA) kuchunguza misimu hiyo na kuona kama kuna baadhi inafaa kusanifishwa.


Journal Identifiers


eISSN: 2591-7013
print ISSN: 2665-0789