Main Article Content

Matumizi ya fasihi katika ukuzaji wa stadi ya tafakuri tunduizi


Laurien Tuyishimire
Wallace Kapele Mlaga

Abstract

Wanafunzi wa vyuo vikuu hawana kiwango cha juu cha stadi ya tafakuri tunduizi kutokana na kwamba hawakupewa misingi mizuri ya kuendeleleza stadi hii kuanzia shule za sekondari (Saleh, 2019). Kutoka na hali hii, tuliona kuna haja ya kutafiti matumizi ya fasihi katika ukuzaji wa stadi ya tafakuri tunduizi katika shule teule za sekondari nchini Rwanda. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya uchanganuzi wa matini, usaili, na ushuhudiaji ili kufanikisha malengo manne ya utafiti: kuchunguza uhusiano uliopo baina ya fasihi na tafakuri tunduizi, kuchunguza hali halisi ya ufundishaji wa stadi ya tafakuri tunduizi katika madarasa ya lugha na fasihi, kubainisha mikakati ya ufundishaji wa stadi ya tafakuri tunduizi na kutoa mfano wa namna stadi ya tafakuri tunduizi inavyoweza kukuzwa kupitia fasihi. Nadharia ya Ujengaji ndiyo iliyoongoza hatua mbalimbali za utafiti ulioibua makala hii. Imebainika kuwa, kutokana na uhusiano wa karibu uliopo baina ya fasihi na tafakuri tunduizi, fasihi ni nyenzo mwafaka ya ukuzaji wa tafakuri tunduizi. Licha ya hivyo, katika madarasa ya fasihi na lugha, walimu wanakabiliwa na changamoto lukuki katika ukuzaji wa tafakuri tunduizi: kukosa uelewa wa kina kuhusu tafakuri tunduizi, kushindwa kujumuisha vema stadi ya tafakuri tunduizi katika masomo yao, na matumizi ya mbinu zisizo mwafaka. Zaidi ya hivyo, makala inabainisha sio tu mikakati mwafaka ya ukuzaji wa tafakuri tunduizi kupitia ufundishaji wa fasihi, bali pia inabainisha namna ambavyo fasihi inaweza kutumika kukuza stadi ya tafakuri tunduizi kupitia mikakati tofauti ikiwemo ujifunzaji unaoegemea kwenye utatuzi wa tatizo.


Journal Identifiers


eISSN: 2591-7013
print ISSN: 2665-0789