Main Article Content
Fasihi ya Watoto ya Kiswahili: mbinu ya kufundishia na kujifunza kusoma na kuandika
Abstract
Katika historia ya fasihi ya Kiswahili, fasihi ya watoto, haina muda mrefu ikilinganishwa na fasihi ya watu wazima. Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa Fasihi ya Watoto ya Kiswahili ilitelekezwa kwa muda mrefu kutokana na wahakiki kutoipa umuhimu unaostahili na hivyo kudharauliwa na wanajamii. Hata hivyo, kuanzia miaka ya 2000 mpaka hivi sasa, kumekuwa na msukumo mkubwa kwa watafiti mbalimbali kufanya tafiti zao kwa kuimakinikia fasihi hiyo. Miongoni mwa mambo yaliyoshughulikiwa ni nafasi ya fasihi katika kumkuza mtoto kisaikolojia, sifa bainifu za fasihi ya watoto, uhusiano wa fasihi ya watoto na umilisi wa kusoma pamoja na mbinu zinazotumika kufundisha fasihi ya watoto. Katika mijadala hiyo, fasihi ya watoto, mahususi kipera cha nyimbo hakijamakinikiwa kama mbinu msingi ya kujifunzia kusoma na kuandika. Jambo hili limeacha pengo la kimaarifa ambalo limezibwa na utafiti uliozalisha makala hii kwa kubainisha ni kwa namna gani fasihi ya watoto (kwa kutumia kipera cha nyimbo), inaweza kutumika kama mbinu msingi ya kufundishia stadi za kusoma na kuandika. Aidha, utafiti uliozalisha makala hii ni wa kitaamuli. Data zilipatikana maktabani kwa kutumia mbinu ya mapitio ya nyaraka. Data zilikusanywa, kuchanganuliwa na kuwasilishwa kwa kutumia Nadharia ya Utabia. Matokeo ya utafiti yamebainisha kuwa fasihi ya watoto, mahususi kipera cha nyimbo ina umuhimu mkubwa katika kufunza stadi za kusoma na kuandika.