Main Article Content
Kuathiriana kwa fonolojia na sintaksia katika lugha ya Kiswahili
Abstract
Makala hii inaangalia jinsi mipaka ya kifonolojia katika kiwango cha nje ya neno inavyoathiriana na sintaksia katika kutoa maana ya tungo za Kiswahili. Inaziba pengo hili, ambalo halijafanyiwa kazi katika isimu ya Kiswahili, kwa kuonesha jinsi ambavyo usarufi na maana ya tungo za Kiswahili hutegemea uhusiano wa muundo wa kisintaksia na muundo arudhi wa tungo hiyo. Makala inaweka bayana kuwa kila tungo huwa na mipaka ya kifonolojia ndani mwake ambayo huweza kubadili muundo au aina ya tungo kisintaksia na hata kubadili maana iliyokusudiwa na msemaji ikiwa itabadilishwabadilishwa. Aidha, inaonesha jinsi maana iliyokusudiwa na msemaji au aina ya tungo iliyokusudiwa hubainishwa na utamkaji wa tungo husika. Data za utafiti huu zimekusanywa uwandani kwa kushuhudia mazungumzo mbalimbali ya watumiaji wa Kiswahili katika nyakati tofautitofauti na sehemu mbalimbali, matini mbalimbali na kwa njia ya mahojiano na watumiaji wa Kiswahili. Mkabala wa kinadharia uliotumika kuchanganua data ni ule wa Nadharia ya Muundo Arudhi. Matokeo yanaonesha kuwa kuna mwingiliano mkubwa baina ya fonolojia arudhi na sintaksia katika kufikisha ujumbe au maana ya tungo iliyokusudiwa.