Main Article Content
Je, Kiswahili nchini Uganda ni lugha ya kigeni au lugha ya pili?
Abstract
Lugha ya pili huweza kuwa lugha rasmi au yenye kuhitajika kutumiwa katika masuala ya elimu, ajira na malengo mengine kama biashara na utalii (Saville-Troke, 2006). Lugha ya kigeni ni lugha inayofundishwa darasani bila kutumiwa katika jamii ambako inafundishwa (Aleidine, 2015). Nchini Uganda, Shirika la Uandaaji wa Mitalaa la “National Curriculum Development Center (NCDC)” linapotoa orodha ya lugha zinazofundishwa katika shule za sekondari, lugha ya Kiswahili na Kiingereza hazibainishwi kama ni lugha za pili (kuanzia sasa Lg2) au za kigeni. Kiarabu, Kifaransa, Kijerumani, Kichina na Kilatini huwekwa kwenye kundi la lugha za kigeni kwa madai kuwa ni lugha za nje ya Uganda. Kiganda, Kinailotiki na Kinyakitara ni miongoni mwa lugha za kikabila zinazofundishwa nchini Uganda. Kiswahili hakijabainishwa kuwa Lg2 au lugha ya kigeni. Kutobainishwa huku husababisha walimu nchini Uganda kuendelea kufundisha Kiswahili bila kuzingatia njia zinazofaa za ufundishaji wa Lg2 au lugha ya kigeni. Makala hii ilinuia kubaini ikiwa Kiswahili nchini Uganda ni Lg2 au lugha ya kigeni ili kuwasaidia walimu kubaini mbinu mwafaka za kukifundisha Kiswahili kwa sababu mbinu za kufundisha Lg2 na lugha ya kigeni wakati mwingine zinatofautiana. Data zilipatikana kwa njia ya mapitio ya nyaraka, ushuhudiaji pamoja na tajiriba aliyonayo mwandishi wa makala hii katika ufundishaji wa Kiswahili nchini Uganda kwa muda wa zaidi ya miaka 15. Matokeo katika makala hii yamebainisha kwamba Kiswahili katika maeneo mengi nchini Uganda ni lugha ya kigeni na katika maeneo machache mno ni Lg2. Hii ni kutokana na sababu kwamba, katika maeneo mengi nchini Uganda, Kiswahili kinafundishwa darasani, hakitumiwi katika shughuli za kijamii.