Main Article Content

Uchanganuzi wa vipashio vya mamlaka katika midahalo ya siasa za uchaguzi wa 2022 nchini Kenya kwenye jukwaa la kidijitali la youtube


Abstract

Makala hii inalenga kutambua mchango wa lugha kama chombo kinachodhihirisha mamlaka katika jamii kwa kuchanganua baadhi ya vipashio vilivyodhihirisha mamlaka katika midahalo ya wakati wa uchaguzi wa 2022 nchini Kenya kama inavyojitokeza katika jukwaa la kidijitali la Youtube. Wanasiasa wana hulka ya kutumia lugha yenye kupendeza kwa wananchi nyakati za kampeni kwa njia ya kipekee ili kubadilisha mawazo yao. Katika harakati hizi, wanasiasa huvuta mamlaka upande wao kwa njia isiyo wazi. Hali hii huwafanya wasikilizaji wengi kukosa kuelewa habari iliyotolewa kwa kutoelewa vipashio vilivyotumiwa katika hotuba hizo, hivyo kufanya maamuzi mabaya kisiasa. Utafiti huu ulizingatia muundo wa kiuchanganuzi kwa kutathmini data za kiuthamano zitakazoelezwa kinathari. Eneo la utafiti ni la kitaaluma. Kundi lengwa la utafiti ni midahalo ya wanasiasa wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka wa 2022 nchini Kenya. Usampulishaji wa kimaksudi ulitumika huku data zikikusanywa kutoka kwenye mtandao wa youtube kwa mbinu ya uchanganuzi wa yaliyomo na kuwasilishwa kimaelezo. Makala hii ilibainisha kuwa japo siasa huwasisimua wananchi na midahalo yake kuwavutia kwa wingi, wengi wao hukosa kuelewa kabisa wayasemayo wanasiasa hawa huku wengine wakipata ufasiri potovu. Data zilizokusanywa zitasaidia katika kudhihirisha sababu za wananchi kutoelewa habari fiche ambazo huwasilishwa na wanasiasa katika midahalo yao, ambacho ndicho chanzo cha wananchi kutoelewa habari hizo na hivyo kufanya maamuzi mabaya kwa kuwachagua viongozi wasiofaa.


Journal Identifiers


eISSN: 2958-1036