Main Article Content

Teknolojia ibuka na ufundishaji wa somo la Kiswahili


Abstract

Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa ni kuchanganua teknolojia ibuka na ufundishaji wa somo la Kiswahili. Katika sekta mbalimbali kama vile afya, benki, biashara, usafiri, utawala, kilimo, ufundi na hata mawasiliano teknolojia za kisasa zinatumiwa. Sekta ya elimu haijaachwa nyuma katika matumizi ya teknolojia hizi. Utafiti huu ulizingatia nadharia ya Piaget inayosema kuwa akili ya mtoto hukua kulingana na mtagusano wake na mazingira. Matokeo ya utafiti huu ni kuwa, Teknolojia ibuka kama vile mtandao, tarakilishi, video, redio, simu, setelaiti, barua pepe, runinga, vipakatalishi, zote zinaweza kutumiwa kurahisisha mawasiliano darasani, kujenga kumbukumbu ya wanafunzi, kuwapa nafasi ya kutafiti mada tofauti, kufurahia kujifunza, kupata uhalisa wa yale wanayojifunza na hata kufanyia mazoezi teknolojia tofauti kwa maandalizi ya ulimwengu wa kazi. Pia idadi ya wanafunzi inaendelea kupanda ikilinganishwa na waalimu wanaotakiwa kushughulikia wanfunzi hawa. Kwa vile Kiswahili ni somo la lazima teknolojia hizi zingekumbatiwa ingekuwa rahisi sana mwalimu kufunza stadi kwa wanafunzi wengi wakati mmoja hata wakiwa katika maeneo tofauti. Teknolojia ibuka huzingatia fahiwa tofauti hasa za kusikiliza na kuona. Redio, epurekoda, runinga, simu za mkononi zinaweza kutumiwa kufunza stadi ya kusikiliza. Tepurekoda, kanda za video, runinga zinaweza kutumiwa kufunza stadi ya kuzungumza. Stadi ya kusoma inaweza kufunzwa kwa kutumia mtandao, vifaa vya kurekodi sauti, nayo stadi ya kuandika inaweza kufunzwa kwa kutumia simu za mkononi, runinga, mtandao au video. Wanafunzi wanaweza kupata ujumbe, ufafanuzi kwa kutafiti mtandaoni. Inatarajiwa kuwa waalimu na wanafunzi wa somo la Kiswahili watazingatia teknolojia ibuka kuelewa somo hili na kupata umilisi wa kutumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano.


Journal Identifiers


eISSN: 2958-1036