Main Article Content

Uchanganuzi wa mielekeo ya wanafunzi kuhusu ufundishaji wa Stadi za Mawasiliano kwa Kiswahili katika taasisi za kiufundi za kitaifa nchini Kenya kwa misingi ya michepuo ya masomo


Abstract

Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa ni kuchanganua mielekeo ya wanafunzi wa kozi za sayansi na sanaa kuhusu ufundishaji wa Stadi za Mawasiliano kwa Kiswahili nchini Kenya. Aidha, kuchunguza visababishi vya mielekeo husika kuhusu umuhimu wa matumizi ya Kiswahili kufundisha stadi za mawasiliano. Muundo wa Uchunguzi Kimaelezo ulitumiwa, huku taasisi 5 za kiufundi za kitaifa na sampuli ya wanafunzi 148 wakishirikishwa katika utafiti. Fomula ya Balian (1988) ya uteuzi wa sampuli ilizingatiwa na ukusanyaji wa data ulitumia kitanga cha mielekeo ya hojaji ya Likert kilichokarabatiwa, maswali ya wazi na dodoso. Waaidha, Zanatepe ya Kichanganuzi Data ya Kitakwimu za Sayansi Jamii (SPSS) kilitumika kuchanganua data. Matokeo yalidhihirisha kuwa, asilimia 2.82 ya wanafunzi 142 waliohusishwa katika uchanganuzi walidhihirisha mielekeo hasi, ilhali asilimia 97.18 walionyesha mielekeo chanya kuhusu ufundishaji wa Stadi za Mawasiliano kwa Kiswahili katika taasisi za kiufundi nchini Kenya. Aidha, wanafunzi wa kozi za sanaa walidhihirisha mielekeo chanya ya chini wakilinganishwa na wenzao wa sayansi. Uchanya huu ulitokana na faida ya utoaji wa huduma uwandani kwa wateja wao waliyoiambatanisha na kuridhia Kiswahili kitumike katika ufundishaji wa stadi za mawasiliano. Kwa mkabala huu, wanafunzi wa taasisi husika waliona umuhimu wa mawasiliano kabambe katika utoaji huduma nyanjani. Hivyo, kuanzishwa kwa ufundishaji wa stadi za mawasiliano kwa kutumia Kiswahili sambamba na Kiingereza kungewasaidia kuchonga maarifa yaliyogusia mawasiliano. Matokeo ya utafiti huu ni ya umuhimu kwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala, Kenya katika utungaji wa sera ya elimu katika taasisi husika.


Journal Identifiers


eISSN: 2958-1036