Main Article Content
Matumizi ya umajazi wa kitashtiti katika usawiri wa wahusika na maudhui katika riwaya: Mfano wa riwaya ya Tumaini
Abstract
Makala hii iliazimia kuhakiki matumizi ya mbinu ya umajazi wa kitashtiti katika kukuza wahusika na kuendeleza maudhui katika riwaya ya Tumaini ya Clara Momanyi. Madhumuni ya karatasi hii ni kuchanganua namna mbinu ya umajazi wa kitashtiti umetumiwa kuwakuza wahusika na kuendeleza maudhui katika riwaya ya Tumaini. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Umuundo. Wataalamu kama Scholes na Olsen wanashikilia mawazo kwamba ni muhimu kutumia Umuundo katika uhakiki wa maandishi ya fasihi kwa sababu lugha na fasihi zina uhusiano mkubwa sana. Matumizi ya Umuundo katika uhakiki wa fasihi hutuelekeza kuitazama fasihi kama mfumo ambao unajumlisha vipengele kama: Fani na maudhui ambavyo huchangia ukamilifu wake. Vipengele hivi huchangiana na kukamilishana katika kazi ya fasihi kama vile riwaya. Nadharia hii ya Umuundo ilitusaidia kuhakiki namna mbinu ya umajazi wa kitashtiti umetumiwa kusawiri wahusika na kuendeleza maudhui katika riwaya ya Tumaini. Ukusanyaji wa data ulifanyika maktabani. Riwaya teule na makala zinazohusiana na mada zilisomwa. Data zilidondolewa, zilichujwa, zilichunguzwa na kisha zilichanganuliwa kwa kutumia majedwali na asilimia ya majina ya majazi ya kitashtiti. Data zilizokusanywa pia zilitumiwa kuhakiki matumizi ya umajazi wa kitashtiti katika kuwakuza wahusika na kuendeleza maudhui katika riwaya ya Tumaini. Pia, tuligundua kwamba mbinu ya matumizi ya umajazi wa kitashtiti yana mchango mkubwa kuwasawiri wahusika na kuyaendeleza maudhui katika riwaya ya Tumaini. Aidha, matokeo ya utafiti huu yatasaidia wahakiki, waandishi, walimu na wanafunzi wa shule za upili na hata vyuoni kuhakiki matumizi ya majina ya kimajazi katika kazi za fasihi andishi. Mbali na kazi hii kuwafaidi wahakiki, matokeo ya utafiti huu yatakuwa na mchango mkubwa katika kuwahamasisha waandishi chipukizi kutumia mbinu ya umajazi wa kitashtiti katika harakati zao za utungaji riwaya.